KANISA LA TANZANIA NA KANISA LA NIGERIA TOFAUTI KATIKA WOKOVU, UAMSHO NA UTHUBUTU
Katika kulinganisha maendeleo ya kiroho kati ya kanisa la Tanzania na Nigeria, hoja kubwa imeibuka kwamba Tanzania bado ipo nyuma kwa kiwango kikubwa linapokuja suala la uamsho, uthubutu na mshikamano wa kanisa.
Nigeria: Historia ya Mababa Wenye Uthubutu
Nigeria imejipatia umaarufu mkubwa katika historia ya injili kutokana na watumishi waliolipa gharama kubwa kwa ajili ya wokovu.
Joseph Ayo Babalola (1930): Alitembea mji kwa mji akihubiri injili na kufufua zaidi ya watu 30.
Benson Idahosa: Anatajwa kufufua zaidi ya watu 24 na kufanikisha uamsho mkubwa unaoheshimiwa hadi leo.
Hadi sasa, majina makubwa kama Papa E.A. Adeboye (RCCG) – kanisa linalokusanya zaidi ya waumini milioni moja duniani, David Oyedepo (Winners Chapel) – ibada ikihusisha waumini 250,000 mara tatu kila Jumapili, na Paul Enenche (Dunamis International Gospel Centre) – anayekusanya zaidi ya waumini 100,000 kwa ibada moja, yanaendelea kushuhudiwa. Aidha, majenerali kama Chris Oyakilome, Ayo Oritsejafor, na Apostle Johnson Suleman wameendeleza mwendelezo wa nguvu za injili Nigeria.
Utafiti unaonyesha siri ya mafanikio yao ni umoja, mshikamano, na uthubutu wa watumishi waliotangulia, hali iliyosababisha kizazi cha vijana kurithi neema na kuendeleza huduma kwa urahisi zaidi.
Tanzania: Changamoto za Mgawanyiko na Ubinafsi
Tanzania pia imeshuhudia uamsho kupitia watumishi kama Mzee Moses Kulola, Mwalimu Christopher Mwakasege, Mchungaji Dustan Maboya, na Askofu Kakobe. Hata hivyo, tofauti kubwa iliyojitokeza ni mgawanyiko miongoni mwa watumishi wa injili.
Mara nyingi watumishi wapya walipoinuliwa, walipingwa na waliotangulia kwa kushutumiwa kuwa “pepo” au “shetani”.
Utamaduni huu wa kusemana na kugawanyika umeendelezwa hadi kizazi cha sasa, jambo linalodhoofisha umoja wa kanisa la Tanzania.
Aidha, historia ya uamsho nchini haijarekodiwa kwa kina, tofauti na Nigeria ambapo kumbukumbu za watumishi na matendo yao zimehifadhiwa na kuenziwa.
Swali linaloibuka ni kama Mungu ataikubalia Tanzania kufikia hata robo ya kile kinachoendelea Nigeria. Wengi wanaona bado anga la Tanzania halijashikiliwa kiroho kwa sababu ya roho ya ubinafsi, choyo na ukosefu wa mshikamano wa kanisa.
Wachambuzi wa kiroho wanasema, bila umoja na uthubutu wa kizazi kipya, ni vigumu kuona Tanzania ikipata ukombozi wa kweli wa kiroho, hata ukombozi wa kisiasa.
Nigeria imekuwa mfano wa taifa ambalo kanisa limeinuka na kushikilia anga za kiroho kwa uthubutu. Tanzania, licha ya kuwa na historia ya watumishi waliotumika kwa nguvu, bado inapambana na changamoto za mgawanyiko na ubinafsi.
Ipo haja ya mjadala wa dhati miongoni mwa Wakristo wa Tanzania, hususani vijana, ili kuamua kama wako tayari kulipa gharama na kupindua meza za mgawanyiko kwa ajili ya injili ya Kristo.
No comments:
Post a Comment